KISWAHILI Form 1 Topic 3

FASIHI KWA UJUMLA
Mada hii ni utangulizi tu juu ya fasihi. Katika utangulizi huu utaelewa dhana ya fasihi, utajifunza juu ya kazi za fasihi katika maisha ya mwanadamu. Utajifunza juu ya tanzu (aina) za fasihi kwa ujumla wake. Kisha utajifunza sifa na dhima za kila tanzu ya fasihi kwa umahususi wake na mwisho utaweza kujifunza juu ya tofauti na uhusiano wa tanzu hizo za fasihi.

Dhana ya Fasihi
Elezea dhana ya fasihi
Fasihi; ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala yanayomhusu binadamu matatizo yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake. (Wamitila, 2004).
Fasili hii imejaribu kufafanua vizuri kile ambacho fasihi inajihusisha nacho, kimsingi fasihi inajihusisha na wanadamu. Vitu vya msingi tunavyoviona katika fasili hii ni kwamba fasihi ni sanaa, na fasihi inatumia lugha lakini zaidi fasihi inajihusisha na wanadamu.
Dhima za Fasihi katika Jamii
Fafanua dhima za fasihi katika jamii
Dhima za fasihi katika jamii ni pamoja na hizi zifuatazo:
  • Kuburudisha jamii:Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.
  • Kuelimisha. Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mabalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.
  • Kuonya jamii. Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
  • Kuunganisha jamii. Fasihi huleta watu katika jamii. Watu huunganishwa kupitia kazi mbalimbali za kifasihi, kwa mfano, kupitia nyimbo, miviga, vichekesho na kadhalika.
  • Kukuza lugha.Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.
  • Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.
  • Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.
Kuna tanzu mbili za fasihi, ambazo ni fasihi andishi na fasihi simulizi.
Dhana ya Fasihi Simulizi
Fafanua dhana ya fasihi simulizi
Fasihi Simulizi ni utanzu wa fasihi ambao unawakilisha sanaa ya lugha inayopitishwa kutoka kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno/masimulizi ya mdomo.
Sifa na Dhima za Fasihi Simulizi
Elezea sifa na dhima za fasihi simulizi
Sifa za Fasihi Simulizi
  • Hupitishwa kwa njia ya mdomo
  • Ufanisi wa sanaa katika fasihi simulizi hutegemea uwezo wa msimulizi, au wahusika.
  • Masimulizi yake yanaweza kuathiriwa na mazingira, hisia na hali
  • Ni mali ya jamii. Hakuna mtu fulani anayemiliki sanaa katika fasihi simulizi.
  • Inaweza kubadilika kutoka kizazi hadi kizazi, au mazingira mbalimbali kwa sababu hutegemea kumbukumbu ya msimulizi.
  • Aghalabu huwa na funzo fulan
Dhima za Fasihi Simulizi
  • Kuburudisha – Hufurahisha na kuchangamsha hadhira
  • Kunasihi- kutolea mawaidha na kuonyesha mwelekeo unaotarajiwa katika jamii.
  • Kuelimisha watu kuhusu vitu mbalimbali hasa mazingira yao
  • Kutambulisha jamii – jamii mbalimbali husifika kutokana na sanaa zao katika fasihi simulizi kama vile nyimbo.
  • Kuhifadhi na kudumisha utamaduni wa jamii
  • Kuunganisha watu – huleta watu pamoja
  • Kukuza lugha – fasihi huimarisha lugha kwa kuwa hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
  • Kuliwaza – hutoa huzuni na kuleta matumaini.
  • Kupitisha muda – wakati mwingine fasihi simulizi hutumika kupitisha muda.
  • Fasihi simulizi ni chombo cha mawasiliano hususani kupitia ngomezi.
Dhana ya Fasihi Andishi
Fafanua dhana ya fasihi andishi
Fasihi Andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno ya maandishi kupitisha ujumbe kwa hadhira.
Kuna tanzu kuu nne za Fasihi Andishi:
  1. Hadithi Fupi – Hii ni kazi ya fasihi andishi yenye kisa kimoja na mhusika mkuu mmoja na maudhui yake sio changamani.
  2. Riwaya –Ni kazi ya fasihi andishi yenye wahusika wengi na muundo changamani ni ndefu na maudhui yake ni mapana.
  3. Tamthilia– ni kazi ya kisanaa yenye muundo wa kiugizikaji inayowasilishwa katika maandishi.
  4. Mashairi – mashairi yakiwa yamechapishwa pia hutambulika kama fasihi andishi.
Sifa na Dhima za Fasihi Andishi
Elezea sifa na dhima za fasihi andishi
Sifa za Fasihi Andishi
  • Hupitishwa kwa njia ya maandishi
  • Ni mali ya mtu binafsi
  • Haiwezi kubadilishwa papo kwa papo
  • Hutumia mbinu za lugha na mbinu za sanaa katika uwasilishaji wake.
Dhima za Fasihi Andishi
  • Kukuza lugha
  • Kuhifadhi kazi ya sanaa katika maandishi
  • Kuburudisha
  • Kuelimisha
  • Kukashifu tabia zisizoandamana na maadili ya jamii
  • Kuonya, kuelekeza, kunasihi
Tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi
Onesha tofauti kati ya fasihi andishi na fasihi simulizi
Zifuatazo ni tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi kama zilivyobainishwa katika jedwali hapa chini:
FASIHI SIMULIZI FASIHI ANDISHI
1. Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo. Huwasilishwa kwa njia ya maandishi
2. Ni mali ya jamii. Kazi andishi ni mali ya mwandishi (na mchapishaji)
3. Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu Fulani Kitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa
4. Huhifadhiwa akilini Huhifadhiwa vitabuni
5. Kazi simulizi hubadilika na wakati Kazi andishi haibadiliki na wakati
6. Huhitaji msimulizi na hadhira yake wawe mahali pamoja wakati wa masimulizi Msomaji anaweza kusoma kitabu cha hadithi peke yake, mahali popote, wakati wowote
7. Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimulia Ni lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma
8. Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi n.k) Hutumia wahusika wanadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Back to top button
Close

Adblock Detected

We've noticed that you're using an adblocker. Our website relies on ads to provide free content. Please consider disabling your adblocker support us. Thank you for your support.